Chanzo Kifo Cha Babu wa Loliondo Chatajwa MwananchiJul 31, 2021

 

                 

             Chanzo Kifo Cha Babu wa Loliondo Chatajwa

MwananchiJul 31, 2021


Summary

Chanzo cha kifo cha Mchungaji Ambilikile Mwasapile(86) kimetajwa aliugua nimonia kali ambayo ilimsababisha kupata tatizo la upumuaji na na homa.

Arusha. Chanzo cha kifo cha Mchungaji Ambilikile Mwasapile (86) kimetajwa aliugua nimonia kali ambayo ilimsababisha kupata tatizo la upumuaji na homa.

Tangu afariki wasaidizi wake na majirani wamekuwa wakieleza kushtushwa na kifo hicho ambacho kimetokea akiwa anaendelea kutoa huduma ya tiba ya kikombe aliyoanza tangu mwaka 2011.


Mchungaji Ambilikile ambaye ataendelea kukumbukwa kwa kuvutia maelfu ya watu ndani na nje ya nchi kati ya mwaka 2011 hadi 2013 kutokana na tiba yake ya kikombe alifariki jana saa 9:45 jioni.


Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Raymond Mangwala amesema kuwa taarifa za awali za madaktari zinaeleza chanzo cha kifo ni nimonia ambapo kwa takriban siku tano alikuwa anaumwa na kupata sindano za masaa.


"Jana asubuhi aliamka vizuri akiendelea na matibabu lakini majira ya saa nane alianza kujisikia vibaya ndipo ilitafutwa gari kutaka kumpeleka hospitali ya Wasso ambaye alitaka,"amesema


Hata hivyo amesema wakiwa wanampandisha gari alijisikia vibaya na kuanza kutapika ndipo walimkimbiza kituo cha afya Chadigodigo na alifika akiwa tayari amefariki.


Baadhi ya wasaidizi wa mchungaji Mwasapile walisema kabla ya kuzidiwa na ugonjwa alikuwa akiendelea kutoa tiba ya kikombe kwa wagonjwa kadhaa ikiwepo wa corona.


Hivi karibuni akizugumza na vyombo vya habari Mwasapile aliomba kupelekewa wagonjwa wa corona kupata tiba kwani hakuna ugonjwa ambao Mungu unamshinda.


"Wiki mbili zilizopita alikuwa vizuri anatoa tiba japo kwa watu mmoja mmoja waliokuwa wanakuja lakini hali yake iliendelea kubadilika," amesema.


James Richard jirani wa Mchungaji huyo amesema hadi anafariki hakuwa na hali mbaya na ameacha mali kadhaa ikiwepo magari, nyumba na kiwanja ambacho alikuwa anaandaa kwa kutolea tiba


"Babu bado alikuwa anasema watu watakuja Samunge maelfu kupata tiba na alipata eneo kubwa ambalo alikuwa anaendelea kuliandaa,"amesema.


Mmoja wa waliowahi kuwa wasaidizi wababu wake Poul Dudui amesema taratibu za mazishi zinaendelea kufanywa kwa uratibu wa Serikali na wanasubiriwa ndugu na watoto wake kujua atazikwa wapi na lini.


James Leyani mkazi wa Loliondo, amesema msiba umetokea wakati kuna janga la corona na kuna chanjo imeanza kutolewa hivyo muhimu watu kusikiliza maelezo ya wataalam wa afya na Serikali.


"Tunakubaliana na tiba za asili na imani lakini sasa muhimu kufuata maelezo zaidi ya wataalam wa afya na Serikali ili kukabiliana na janga hili,"amesema.


Mwisho.

Comments

Popular posts from this blog

Mtaka: Hali si nzuri Dodoma, chukueni tahadhari dhidi ya Covid-19

ZaidiKitaifa VIDEO: DC Handeni aonya wanaonyonya maziwa ya wake zao