Skip to main content

Haji Manara

 

            

                       


Kilichomng’oa Manara Simba hiki hapa

THURSDAY JULY 29 2021
manara pic
By Mwandishi Wetu

MWISHO wa zama. Kama utani Haji Manara leo hii amebaki kuwa mwanachama na shabiki tu wa Simba, baada ya kupigwa chini na nafasi yake kupewa aliyekuwa ofisa habari na kaimu katibu mkuu wa klabu hiyo, Ezekiel Kamwaga.

Simba jana ilitangaza mabadiliko yaliyotarajiwa baada ya mzozo ulioibuka siku chache kabla ya mechi ya fainali ya Kombe la ASFC kati ya timu hiyo na Yanga uliochezwa Jumapili iliyopita mjini Kigoma.

Inaelezwa uhusiano usioridhisha na wanahabari, baadhi ya wadau wa soka na utovu wa nidhamu kwa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez ni sababu zilizochangia kwa kiasi kikubwa kumng’oa Manara ndani ya nafasi hiyo iliyompatia umaarufu mkubwa hasa dhidi ya Yanga.

Licha ya kuvumiliwa kwa muda mrefu na klabu hiyo, kukithiri kwa migogoro ya mara kwa mara baina ya Manara na wanahabari za michezo katika siku za hivi karibuni kunaonekana kuifanya Simba ichukue uamuzi mgumu wa kuridhia ombi lake la kujiondoa katika nafasi aliyoitumikia tangu 2014.

Miongoni mwa wanahabari za michezo ambao kwa nyakati tofauti wamekwaruzana na Haji Manara ni Shaffih Dauda, Prisca Kishamba, Yusuph Mkule, Maulid Kitenge, Abdul Dunia na Ahmed Kivuyo. Pia amewahi kukwazana na maofisa habari wenzake Zaka Zakazi (Azam FC), Hassan Bumbuli (Yanga) na Masau Bwire wa Ruvu Shooting.

Lakini kitendo cha Manara kutoa kauli kumshambulia Barbara kupitia sauti iliyosambaa katika mitandao ya kijamii kimemuweka matatani zaidi kwa mabosi na mashabiki wa Simba. Katika sauti hiyo, alisikika akimtuhumu Barbara kuwa amekuwa akimfanyia visa na kumlaumu kwa kuhujumu timu.

ADVERTISEMENT

“Mimi sinunuliki kwa thamani yoyote ya pesa, unataka kunifedhehesha mimi, watu gani mimi hata gari yangu ilipita Posta, Kigamboni mimi naendaje, kwa hiyo mimi nitoke Posta niende Kigamboni kwenye kambi ya wale,” alisikika Manara.

Sauti hiyo ya Manara akimshambulia Barbara ilionekana kukwaza wengi na mmojawapo ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Zacharia Hanspope aliyesema ofisa habari wao huyo alionyesha utovu wa nidhamu kwa kurekodi na kusambaza sauti hiyo.

“Amekosa maadili kama hakuridhika na alichofanyiwa na CEO na yeye ni binadamu kama wengine anaweza kuwa anakosea, lakini sio kwa namna aliyoitumia angeweza kwenda ngazi za juu apeleke malalamiko kwenye bodi,” alisema Hanspope

Kauli hiyo ya Hanspope ni kama iliichochea Bodi ya Wakurugenzi ya Simba chini ya mwenyekiti Mohammed Dewji kuamua kumuweka kando Manara na kumtangaza Ezekiel Kamwaga kuwa atakaimu nafasi hiyo kwa muda wa miezi miwili.

“Tunamshukuru kwa maneno aliyoyatumia kutuaga Wanasimba katika kundi la viongozi wa Simba (Simba HQ), kwa kazi aliyoifanyia klabu katika kipindi alichoshika nafasi na inamtakia kila heri katika shughuli zake,” taarifa hiyo ya klabu ilisomeka hivyo.

“Mara baada ya kukamilika kwa maboresho ya idara ya habari na mawasiliano na Idara nyingine, klabu itatangaza fursa mbalimbali za ajira katika kipindi cha wiki chache zijazo.”

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wadau mbalimbali wa soka wamesema hawashangazwi na uamuzi huo wa Simba.

“Sio jambo jema kwa wana michezo kutokana na ukweli usiopingika kuwa Haji ameitengeneza ‘brand’ (nembo) ya Simba kuwa kubwa lakini kunapotokea migongano ya kimaslahi kwenye taasisi lazima mmojawapo awajibike.

“Hivyo Simba wanapaswa kutafuta mtu ambaye atakuwa ni zaidi ya Manara ili baadaye isitokee mfanano wa Manara na mwingine kitu ambacho watakuwa wakikiishi kwa sasa kutoka kwa mashabiki zao,” alisema Mtendaji Mkuu wa zamani wa Azam FC, Saad Kawemba

Mchambuzi wa soka, Alex Kashasha alisema alitegemea jambo kama hilo kutokea ili kulinda sura ya taasisi.

“Hayo ndiyo maisha binafsi, imetokea kwa wakati sahihi kutokana na miiko ya taasisi yao imeona inatosha kwake kuendelea kuwepo kutokana na mgogoro ambao umetokea na mabosi wake, hivyo kwa Simba kuachana naye ni jambo la kawaida kwa kuwa Simba ni kubwa kuliko mtu yeyote,” alisema.

Rais wa zamani wa Simba, Ismail Rage alisema: “Nadhani viongozi wanajua zaidi kuhusiana na hili, lakini pia kwa kawaida unapokuwa na mgogoro na mabosi wako unategemea itatokea nini? Hivyo mabosi wanajua sababu nyingine za kuachana naye zaidi ambazo ninazifahamu.”

ADVERTISEMENT

Comments

Popular posts from this blog

Mtaka: Hali si nzuri Dodoma, chukueni tahadhari dhidi ya Covid-19

ZaidiKitaifa VIDEO: DC Handeni aonya wanaonyonya maziwa ya wake zao